Tukizingatia kufanya usafi kipindupindu kitapita mbali

Image result for uchafu sokoni

HIKI ni kipindi cha mvua za masika kwa karibu nchi nzima. Mvua ni baraka kwa watu, lakini wakati mwingine huwa kinyume cha baraka hizo kwani zinaweza kuambatana na athari kama mafuriko yanayosababisha uharibifu wa mali na hata kupoteza maisha ya watu.
Kadhalika, mvua zisipotazamwa kwa umakini, huwa kichocheo kikubwa cha magonjwa ya mlipuko kama kipindipindu na homa ya matumbo maarufu kama taifodi. Ikumbukwe kuwa, baada ya kuingia madarakani Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, alibadili shamrashamra zilizokuwa zifanyike katika sherehe za uhuru wa Tanganyika, Desemba 9, 2015 na kuzifanya zitumike kuwa kampeni ya usafi nchi nzima siku hiyo.
Uamuzi wa Rais ulilenga badala ya kutumia nguvu kubwa na pesa nyingi kufanya sherehe huku eneo la afya likiwa tete kutokana na hali ya kipindupindu ilivyokuwa, Rais aliona ni busara kutumia rasilimali hizo kuzuia ugonjwa huo na mambo mengine yenye manufaa zaidi. Zuio pekee la ugonjwa wa kipindupindu ambalo ni la kisayansi ni usafi wa mazingira na chakula.
Ugonjwa wa kipindupindu huenezwa kwa njia ya uchafu hasa kula kinyesi aidha kupitia chakula, maji au hata ukosefu wa usafi wa mikono kabla na baada ya kula. Hiyo ndiyo iliyoifanya hata Serikali mkoani Dar es Salaam kuweka utaratibu wa wananchi kufanya usafi maalumu katika maeneo yao ya kazi na makazi kila Jumamosi alfajiri hadi saa 4 asubuhi.
Kimsingi, ili kuhakikisha ugonjwa wa kipindupindu na magonjwa mengi ya mlipuko yanapigwa vita jijini Dar es Salaam na nchini kote, yapo mambo muhimu yanayopaswa kufanywa.
Kila mmoja tangu ngazi ya familia azingatie usafi wake binafsi na mazingira yanayomzunguka kwa kula na kunywa vitu vilivyoandaliwa na kuhifadhiwa katika mazingira salama na safi kiasi cha kutosha.
Maji yachemshwe, yachujwe na kuhifadhiwa katika usafi. Vyakula viliwe kupitia mikono na vyombo visafi huku kila mmoja akizingatia kunawa kwa maji ya moto na sabuni kila atokapo chooni, kabla na baada ya kula chochote.
Mifereji isiachwe wala kuruhusiwa kutuamisha maji na kadhalika, takataka zinazokusanywa siku za Jumamosi, ziondolewe haraka barabarani na katika malundo ili zisiwe kero inayoalika na kusambaza nzi wenye viini vya ugonjwa huo.
Jamii ikumbuke kuwa, nzi ndiyo wasambazaji wakubwa wa ugonjwa wa ugonjwa huo unaoambukizwa kupitia vimelea vya bakteria vijulikanavyo kitaalamu kama “vibrio cholerae.”
Namna nyingine ya kudhibiti ugonjwa huu, ni wataalamu wa afya nchi nzima kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wachukue tahadhari zaidi huku Serikali ikihakikisha kuna dawa za kutosha kwa ajili ya kinga na tiba linapotokea tatizo hilo.
Wataalamu wa afya washirikiane na viongozi katika maeneo ya watu katika kuelimisha jamii kuhusu kinga, dalili na tiba za ugonjwa wa kipindupindu. Waelimishwe dalili hizo ili wanapoziona, wasichelewe na hata kufikiria miujiza au kuingiza imani za ushirikina, bali wawahi katika zahanati, vituo vya afya au hospitali kupata matibabu sahihi. Kimsingi, tukizingatia usafi ugonjwa wa kipindupindu tutausikia kwa mbali kama historia.

(source Habari leo}

Comments

Popular posts from this blog

Nchi 10 zenye mazingira safi duniani.

Magonjwa yanayoongoza kusababisha vifo Tanzania

Maji na usafi wa Mazingira